Tuesday, July 6, 2010

Wanamuziki zaidi ya 200 wafa nchini




TANZANIA imefiwa na wanamuziki zaidi ya 200 waliofariki kutokana na sababu mbalimbali
ikiwemo magonjwa na ajali.

Takwimu hizi hazijatolewa na Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo wala Chama cha muziki
wa Dansi nchini CHAMUDATA, bali mwanamuziki mkongwe nchini, Yusuph Subwa.

Mwanamuziki huyo ambaye amewahi kuzipigia bendi mbalimbali nchini zikiwemo Afro 70 ya
marehemu Patrick Balisidya na Super Matimila ya Dr Remmy Ongala, amesema kuwa yeye
mwenyewe amewahesabu na tayari wamefika 200.

Subwa ambaye kwa sasa analiongoza kundi la Exel 1 lenye makao makuu yake Temeke Sokota,
ametunga kibao cha kuwakumbuka marehemu wote ambao ni wanamuziki.

"Katika hicho kibao nimewataja wanamuziki wote waliofariki nchini tangu enzi hizo, katika
karatasi yangu nina wanamuziki 200 hao wa Kitanzania tu waliofariki na wote ninawataja kwenye nyimbo yangu," alisema.

Amesema kuwa hapo hajataja wanamuziki wa Kikongomani ambao walikuwa na bendi mbalimbali nchini ambao wamefariki dunia na kuzikwa hapa hapa nchini.
"Mimi hao sikuwataja, ila nimewataja Watanzania tu ambao kusema kwei waliipaisha nchi yetu
kwenye ramani ya muziki nchi za nje, amini usiamini wako 200 na kama nikiendelea kuwakumbuka waongezeka kidogo," alisema.

Subwa ambaye ni mpiga drums, amesema kuwa katika historia ya maisha yake wamesafiri nchi
mbalimbali za nje hasa bara la Ulaya akiwa bendi ya Super Matimila ambapopia katika ziara yao
wameshawahi kupiga jukwaa moja na hayati Franco wa Kongo na Manu Dibango wa Cameroon
na kupata wasaa wa kubadilishana nao mawazo wakiwa pamoja na Remmy aliyeokoa kwa sasa.

No comments:

Post a Comment