MWENYEWE anasema mwaka 2005 kura 'hazikutosha', ndio maana hakuweza kuteuliwa kuwa mgombea wa Ubunge Jimbo la Same Mashariki kupitia chama tawala, CCM.
Hata hivyo, anasema katika uchaguzi mkuu ujao ambao mbio zake zimeanza rasmi ndani ya chama hicho, ana imani kubwa ya kura zake kutosha na kupitishwa kuipigania CCM katika kinyang'anyiro cha uchaguzi mkuu utakaofanyika nchini nzima Oktoba mwaka huu.
Majina yake kamili ni Naghenjwa 'Nagy' Livingstone Kaboyoka, mwanaharakati wa maendeleo ya jamii, mmoja wa wagombea waliotangaza nia ya kutaka kuwania kiti cha ubunge cha jimbo la Same Mashiriki ambalo kwa sasa kinashikiliwa na Anne Kilango Maceleca.
Mwanamama huyo mwenye shahada ya pili na masuala ya Maendeleo ya Jamii aliyoipata nchini Uingereza na mtaalam wa lugha mbalimbali za kimataifa, alisema ana imani uchaguzi mkuu wa mwaka huu atapata fursa kuiwakilisha CCM na kushinda kiti cha jimbo hilo.
Alisema kitu kinachompa jeuri ya kuamini kuwa ataibuka ushindi ni utaratibu mpya wa mfumo wa upigaji kura ndani ya CCM katika uteuzi wa wagombea wa chama hicho, pia uungwaji mkono aliopata toka kwa wakazi wa jimbo hilo tangu ulipomalizika uchaguzi wa mwaka 2005.
"Pamoja na kutambua upinzani utakuwa mkubwa ndani ya CCM, lakini taratibu na kanuni mpya zinazojumuisha wingi wa wapiga kura kura tofauti na zamani ilipokuwa kikundi kidogo tu cha watu ndicho kinachonipa nguvu ya kushinda," alisema Nagy.
Alisema pamoja na kwamba tayari wanachama wenzake kadhaa wameshajitokeza kutaka kuwania kiti hicho hicho akiwemo mtetezi, Anne Kilango, hana hofu yoyote kwa vile anajiamini uzoefu wake katika kujitolea katika huduma za maendeleo ya jamii ni silaha kubwa kwake.
Mwanamama huyo aliyeolewa na mwenye watoto watatu, alisema yeye ni mwenyeji wa jimbo hilo na kipindi cha nyuma kabla ya kwenda nje ya nchi kulitumikia taifa lake, alisaidia mno kuanzishwa miradi mbalimbali ya kijamii ambayo iliwasaidia wakazi wa jimbo hilo.
Alisema kutokana na hilo na dhamira yake ya kweli ya kuwaletea maendeleo wakazi wa Jimbo hilo waliokata tamaa ya kimaisha kutokana na umaskini mkubwa walionao licha ya kuwa katika jimbo lenye utajiri wa rasilimali, anaamini hakuna wa kumdondosha.
Nagy, aliyewahi kufanya kazi Ubalozi wa Tanzania nchini Denmark, alisema kikubwa atakachozingatia iwapo atachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo, ni kuwashirikisha wananchi katyika kujiletea maendeleo ili kuondoka na hali ya umaskini walionao.
"Nimeamua kujitokeza kuwania Ubunge wa Jimbo la Same Mashariki, kubwa ni kuhakikisha
rasilimali zilizopo jimboni humo ziweze kuwainua wananchi kiuchumi kwa kuwashirikisha katika miradi kutokana na kubobea katika shughuli za maendeleo ya jamii," alisema.
Aliongeza kuwa, anaamini rasilimali zilizopo katika jimbo hilo zikitumiwa vema kwa kuwashirikisha wananchi zinaweza kuwaondolea umaskini na kuwaletea maendeleo yanayoweza kulinganishwa na majimbo mengine ya wilaya yao ya Same ambayo yapo juu kwa sasa.
Alisema mbali na kuwashirikisha wananchi katika miradi mbalimbali ya kimaendeleo na uchumi, lakini pia ataelekeza nguvu zake katika kuboresha mazingira na huduma za kijamii ili kuwafanya wakazi wa jimbo hilo kuifaidi 'keki' ya Uhuru wa Tanzania.
"Ni aibu kwa mkulima wa jimbo hili lenye rasilimali nyingi kutembea karibu kilomita 10 kwa miguu kupeleka mazao yake sokoni, sisemi kama hakuna kilichofanyika, ila kunahitajika mtu wa kuleta mabadiliko ya kweli na sio kupiga kelele tu," alisema Nagy, Afisa Utumishi wa Hospitali ya Kinondoni.
Kuhusu vita dhidi ya ufisadi, alisema haipaswi kufanywa kwa makelele bila utekelezaji wa vitendo ili kukomesha matendo hayo na kuwasaidia wananchi kuinua kimaendeleo na uchumi.
"Kelele zinazopigwa kama hazileti tija na ufanisi wa kweli, wananchi wanaweza wasiwaelewe wanaovipigana kwa sababu hawaoni mabadiliko katika maisha yao ya kila siku, hivyo ni vema tushikamane na kuupiga vita ufisadi kikwelikweli na sio kupiga blabla tu," alisema Nagy.
Alipoulizwa haoni kama atapata upinzani mkubwa kutokana na watu waliojitokeza hadi sasa katika kuwania jimbo hilo akiwemo anayekishikilia kiti hicho, Nagy alisema hahofii mtu yeyote kwa vile anajiamini ana uwezo wa kushinda na kuwaongoza wakazi wa jimbo hilo.
"Pamoja na kufahamu changamoto zilizopo, lakini safari hii nimejipanga vema na simuhofii yeyote kwa sababu mahakimu wetu ni wananchi ambao ndio walionisihi kugombea tangu mwaka 2005, ingawa nilikwamishwa katika kura za maoni na kwa utaratibu wa sasa naamini nitashinda," alisema.
Mwanamama huyo alizaliwa Agosti 8, 1949 na amesoma hadi kufikia ngazi ya Chuo Kikuu na amewahi kufanya kazi sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi, akijishughulisha na masuala ya maendeleo ya kijamii, kama miradi ya maji, afya na mengineyo.
No comments:
Post a Comment