Tuesday, July 6, 2010

Snake Boy, Maugo kuzidunda PTA






PAMBANO litakalomrudisha tena ulingoni bingwa wa zamani wa ngumi za kulipwa nchini na
Duniani, Rashid Matumla 'Snake Boy' dhidi ya Mada Maugo litarajiwa kupigwa kwenye ukumbi
wa PTA, Temeke jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Rais wa Organaizesheni ya Ngumi za Kulipwa nchini, TPBO, Yasin Abdallah
'Ustaadh', pambano hilo lisilo la kuwania mkanda wowote litafanyika Julai 18 mwaka huu.

Rais huyo alisema pambano hilo la raundi nane, limepangwa kufanyika kwenye ukumbi huo wa
PTA kutokana na kuwezesha mashabiki wa ngumi jijini kuweza kulishuhudia kwa raha zao
sambamba na michezo mingine ya utangulizi itakayolisindikiza pigano hilo maalum.

"Lile pambano linalosubiriwa kwa hamu kati ya Snake Boy na Maugo litafanyika kwenye ukumbi
wa PTA na maandalizi kwa ujumla yanaendelea vema, ikiwemo kuthibitisha kwa mabondia
watakaopamba ulingoni kulisindikiza siku hiyo ya Julai 18," alisema Ustaadh.

Ustaadh, alisema mpambano huo umeandaliwa maalum kwa nia ya kumaliza ubishi baina ya
mabondia hao wawili ambao wamekuwa wakitambia kwa muda mrefu.

"Pamoja na lengo la kukuza na kuendeleza mchezo wa ngumi, lakini pia kubwa ni kumaliza ubishi
baina ya mabondia hao wawili ambao wamekuwa wakitambiana kila kukicha, kila mmoja
akitamba ni mkali zaidi ya mwenzake," alisema.

Alisema pambano hilo la uzito wa kilo 72, limeanza kuamsha hisia za wapenzi na mashabiki wa
ngumi wanaotaka kujua nani zaidi baina ya mabondia hao wawili.
Ustaadh aliwaomba wadau mbalimbali wa mchezo wa ngumi kujitokeza kulidhamini pambano
hilo kwa nia ya kurejesha nguvu na hamasa katika mchezo huo wa ngumi.

"Wakati mabondia wakiendelea kujifua kwa ajili ya kuonyeshana umwamba ulingoni, tulikuwa
tunawaomba wadau na watu mbalimbali kujitokeza kulidhamini pambano hilo, ili kuongeza
hamasa na ushindani baina yao," alisema.

No comments:

Post a Comment