Tuesday, July 6, 2010

Mhazini Simba 'awekwa' kiporo





UONGOZI wa klabu ya soka ya Simba umeshindwa kumtangaza Mhazini Mkuu wa klabu hiyo
kama ulivyokuwa umeahidi kwa maelezo kwamba hata akiteuliwa hatakuwa na kazi za kufanya
kwa sasa.

Hata hivyo uongozi huo umesisitiza kuwa muda muafaka ukifika mtu wa kushika nafasi hiyo
atateuliwa kuungana na Afisa Utawala na Msemaji wa klabu ambao tayari wameshaanza kazi
ndani ya klabu hiyo.

Mwenyekiti wa Simba, Ismail Rage, alisema kamati yao ya utendaji imeona ni vema kuachana na
uteuzi wa mhazini mkuu kwa sasa kwa vile majukumu mengi ndani ya klabu yao yapo kwa Afisa
Utawala anayekaimu pia Ukatibu Mkuu na msemaji mkuu walioteuliwa hivi karibuni.

Rage, alisema hata kama watamteua hivi sasa mhazini hatakuwa na kazi za kufanya kama ilivyo
kwa Evodius Mtawala ambaye ni Afisa Utawala au Cliford Ndimbo aliyerejeshewa cheo chake cha usemaji mapema wiki hii.

"Ni kweli tulikuwa na nia ya kuteua mhazini mkuu, lakini tumeona wawili hawa wa kwanza ndio
muhimu na wanaohitajika haraka na muda ukifika wa kumtaka Mhazini tutamteua," alisema Rage.

Rage aliongeza kuwa, kama alivyoahidi akiingia madarakani ni kwamba ndani ya siku zake 100
zitakazokamilika Agosti 17, ikiwa ni siku nne kabla ya kuanza kwa ligi kuu msimu huu, kila kitu
kitakuwa kimeenda sawa na hivyo wanachama wa Simba hawapaswi kuwa na shaka nae.

"Wenyewe wanaona mambo yanavyoenda vema, jengo sasa linakarabatiwa, tayari tuna afisa
utawala na msemaji, uwanja wa mazoezi upo na bado kuna mengine yanakuja kabla hata zile siku
100 hazijakamilika," alisema Rage.

Rage aliwaomba wanachama wa Simba wakati akiingia madarakani Mei 9 kuwa wampe siku 100
kuweza kuibadilisha klabu yao toka katika hali mbaya iliyokuwa nayo hadi kurejea enzi zake na

moja ya vitu alivyotilia mkazo ni kuimarisha uongozi na kulikarabati jengo vituo vilivyofanyika.

No comments:

Post a Comment