Tuesday, July 6, 2010

Vita ya Uholanzi na Uruguay ni kesho * Ni katika mechi ya nusu fainali ya WOZA 2010, Ujerumani, Spain kumalizana J'5



CAPE TOWN, Afrika Kusini
BAADA ya kufanikiwa kuzing'oa 'kimiujiza' timu za Brazil na Ghana katika hatua ya robo fainali, Uholanzi na Uruguay usiku wa kesho zinatarajiwa kuonyeshana kazi kwenye pambano la Nusu Fainali ya kwanza ya michuano ya Fainali za Kombe la Dunia 2010 zinazofanyika nchini hapa.
Pambano hilo litakalochezwa kwenye dimba la Green Point, uliopo Cape Town, linatajaliwa kuwa kali kutokana na soka la lililoonyeshwa na timu zote katika mechi za michuano ya mwaka huu.
Uholanzi inayofahamika kama 'The Orange' wanakutana na Uruguay baada ya kuisambaratisha Brazil kwa kipigo cha mabao 2-1 na kufikia rekodi yao ya kucheza hatua hiyo kwa mara ya nne baada ya kufanya hivyo fainali za mwaka 1974, 1978 na 1998.
Ikiwa na wachezaji wenye vipaji na uwezo mkubwa wa kusukuma gozi kama Robin Van Perse, Arjen Robben, Wesley Sneijder, Nigel de Jong, Mark van Bommel, Giovanni van Bronckhorst, Dirk Kuyt na wengineo leo itakuwa na kazi kubwa kuweza kuizuia Uruguay iliyoing'oa Ghana.
Kama ilivyo kwa Uruguay, ambayo haijaonja kipigo chochote katika michuano ya WOZA 2010, Uholanzi itataka kushinda mechi hiyo na kufuzu fainali ikirejea mafanikio ya fainali mbili mfululizo za mwaka 1974 na 1978, iliyoishia kulikosa kombe kwa Ujerumani na Argentina.
Pengine mwaka huu Uholanzi itapenda sio kufuzu fainali tu bali kuvunja mwisho wa kutotwaa taji hilo licha ya kuwa nchi yenye wachezaji wenye uwezo miubwa kisoka duniani.
Hata hivyo itawabidi Uholanzi wafanye kazi ya ziada mbele ya Uruguay ilifuzu hatua hiyo ya fainali ikiwa ni baada ya miaka 40, kwa kuing'oa wawakilishi wa Afrika, Ghana kwa mikwaju ya penati 4-2 kufuatia kumaliza dakika 120 zikitoka sare ya bao 1-1.
Uruguay yenye mshambuliaji mwenye njaa ya magoli, Diego Forlan, Luis Suarez, Alvaro Pereira, Diego Perez na wengine bila shaka haitakubali kirahisi kuwa ngazi ya kuwafusha wapinzani wao fainali wakati wenyewe wanapenda kufika huko kurejea kurejea mafanikio ya fainali za 1930 na 1950 waliibuka mabingwa wa fainali hizo.
Hivyo pambano hilo la kesho ni gumu kutabirika kutokana na rekodi za timu zote mbili ambazo kila mmoja inampa nafasi sawa ya kuibuka na ushindi na kutinga fainali kusubiri kucheza na mshindi wa mechi nyingine ya hatua hiyo inayochezwa Jumatano kati ya Ujerumani na Spain.
Ujerumani ilipata nafasi hiyo baada ya kuisasambua Argentina kwa mabao 4-0, huku Spain ikipata ushindi 'kiduchu' wa bao 1-0 dhidi ya Paraguay.
Mechi ya fainali za WOZA 2010 itachezwa siku ya Jumapili kwenye dimba la Soccer City, Johannesburg.

No comments:

Post a Comment