KAMPUNI ya usambazaji wa filamu nchini ya Steps Entertainment imejitosa kwenye muziki wa Injili na sasa iko mbioni kutoa DVD mbili za miondoko hiyo moja ikimjumuisha nyota wa zamani wa dansi, Kitenzogu Makassy 'Mzee Makassy'.
Mkongwe huyo aliyetamba na bendi mbalimbali za dansi ikiwemo Makassy Band, kwa muda mrefu amejitosa kwenye muziki wa Injili, ambapo Steps imeijumuisha kazi yake katika DVD iitwayo Amen Gospel Colletion inayotarajiwa kutoka sambamba na Ebenezer Collection Vol.1.
Kwa mujibu wa Steps, DVD hizo kila moja itakuwa na jumla ya nyimbo tisa za nyota wa miondoko hiyo wakiwemo Jane Misso, Christina Shusho, Bonny Mwaitege na wengineo.
Taarifa ya Steps inasema katika DVD ya Amen, mbali na Mzee Makassy, albamu hiyo ina nyimbo kama 'Hakuna kama Yesu' wa Christina Shusho, 'Lango ni Yesu'- Jane Misso, 'Mimi Siyawezi-Abedy Ngosha na 'Bwana ndio Mchungaji' ulioimbwa na Solomoni Mukubwa.
Katika albamu ya pili ya Ebenezer Collection Vol.1, ina nyimbo za wakali kama Bonny Mwaitege, Abiud Mashari, Neema Mwaipopo, Ambwene Mwasongwe na wengineo na zote zintarajiwa kutoka kabla ya sikukuu ya Krismasi.
"Steps tupo mbioni kuingiza mtaani albamu mbili za muziki wa Injili zinazohusisha nyota wa miondoko hiyo zitakazokuwa na nyimbo tisa kila mmoja, ambapo moja inafahamika kwa jina la Amen Gospel Collection na nyingine Ebenezer Collection Vol. 1," taarifa hiyo ya Steps inasomeka hivyo.
No comments:
Post a Comment