Friday, December 9, 2011

Kanumba sasa ni Big Daddy



BAADA ya kutamba na 'Because of You', nyota wa filamu nchini, Steven Kanumba 'The Great', anajiandaa kupakua kazi nyingine mpya itwayo 'Big Daddy'.
Filamu hiyo mpya ya Kanumba, imewashirikisha wasanii tofauti wakiwemo wakongwe na chipukizi ambao wamefanya kazi kubwa, kwa sasa ipo kwenye foleni kabla ya kuachiwa sokoni.
Kwa mujibu wa Kanumba, kazi hiyo yenye ubora wa hali ya juu itaingia sokoni wiki tatu zijazo, ingawa yupo 'chimbo' kuandaa kazi nyingine kwa ajili ya kufungia mwaka.
Mbali ya Kanumba, ndani ya filamu hiyo amecheza na wasanii kama Jamila Jaylawi, Jalilah Jaylawi, Cathy Rupia, Abdul Ahmed, Patchou Mwamba na wengine.
"Si kazi ya kuikosa kuiona kwa namna simulizi lake lilivyo na inavyosisimua," alisema Kanumba.
Katika hatua nyingine, msanii mwingine mkali wa fani hiyo, Mohammed Nurdin 'Chekibud' amepakua kazi iitwayo Azma ambayo inatarajiwa kutoka katikati ya mwezi huu ikiwashirikisha nyota kadhaa akiwemo Kulwa Kikumba 'Dude'.
Filamu hiyo inayohusiana na mambo ya mapenzi, ipo foleni kabla ya kuingizwa sokoni, pia imewashirikisha waigizaji kama Zuwena Mohammed 'Shilole', Snura Mushi na wengine.
Chekibud, amewataka mashabiki wake kujiandaa kuishuhudia kazi hiyo aliyodai ni moja kati ya filamu za kufungia mwaka 2011 kutokana na ubora iliyonayo kuanzia hadithi, mandhari na washiriki walivyoicheza.

No comments:

Post a Comment