
BAADA ya kimya cha muda mrefu hatimaye mmoja wa wanamuziki waanzilishi wa bendi ya Twanga Pepeta, Ally Akida, amejiunga na bendi inayokuja kwa kasi katika anga za muziki wa dansi ya Extra Bongo.
Mkurugenzi wa bendi hiyo, Ally Choki alisema kuwa amemuongeza Akida kwa vile ni mwanamuziki kiraka ambaye anamudu kupiga gita lolote na kwamba hata mmoja anapopata dharura kazi itaendelea kama kawaida.
"Ninaujua uwezo wa Ally Akida ndio maana tumemchukua ili ajiunge na bendi yetu, kwani kwa muda mrefu kidogo alikuwa anafanya shughuli zake tu baada ya kuachana na Twanga Pepeta," alisema Choki.
Alisema kwamba atakuwa na msaada mkubwa kwenye bendi hiyo ambayo kwa sasa inaendelea na kazi ya kujitambulisha ndani na nje ya Dar es Salaam huku pia ikiwa mbioni kukamilisha albamu ya pili.
Alisema kuwa ingawa mwanamuziki huyo hajambulishwa rasmi kwa wapenzi wa bendi hiyo, ana uhakika kwamba wale ambao wamekuwa wakihudhuria maonyesho ya Extra Bongo wameshamuona akifanya vitu vyake.
"Tuna sababu zetu za msingi za kutomtambulisha rasmi, lakini wakati mufaka ukifika tutafanya mara baada ya kukamilisha mipango ya kuongeza wanamuziki wengine kazi ambayo bado inaendelea,"alisema.
Alifafanua kuwa mipango hiyo ikikamilika, Extra Bongo itawatambulisha wanamuziki wote wapya akiwemo Ally Akida aliyejiunga na bendi hiyo hivi karibuni ikiwemo pia mpiga tumba mpya John Ngosha.
John Ngosha ni mtoto wa mwanamuziki wa zamani wa bendi ya DDC Mlimani Park 'Sikinde', Charles marehemu John Ngosha.
Extra Bongo ilianza kwa albamu ya 'Mjini Mipango' na sasa imekamilisha nyimbo za albamu ya pili zikiwemo za 'Fisadi wa Mapenzi', 'Watu na Falsafa', 'Mtenda Akitendewa', 'Mashuu', 'Neema' na nyinyine nyingi.
Nyimbo hizo zimekuwa zikiporomoshwa kwenye maonyesho ya bendi hiyo likiwemo la kila Jumamosi ambalo hufanyika katika ukumbi wa Meeda Club uliopo Sinza-Mori, jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment