

UPINZANI wa wachezaji Emmanuel Okwi wa Uganda na Haruna Niyonzima wa Rwanda wanapokuwa katika klabu zao za Simba na Yanga, utarejea tena leo wakati mataifa hayo mawili yatakapopambana katika mechi ya fainali ya Kombe la Chalenji kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuanzia saa 9:15 alasiri.
Mechi hiyo itatanguliwa na pambano la kusaka mshindi wa tatu baina ya mabingwa wa mwaka jana Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars' dhidi ya Sudan litakaloanza saa 7:00 mchana. Awali michezo hiyo ilipangwa kuanza saa 8:00 mchana kwa mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu na saa 10:00 jioni kwa mchezo wa fainali lakini Baraza la Vyama vya Michezo la nchi za Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) jana lilirekebisha ratiba hizo.
Okwi, mbali na ushindani dhidi ya hasimu wake wa Yanga, Niyonzima, pia atakuwa akichuana na mshambuliaji ghali wa APR ya Rwanda, Olivier Karekezi mwenye magoli matano katika mbio za kuwania tuzo ya kiatu cha dhahabu ya mfungaji bora. Okwi ameifungia Uganda magoli manne katika michuano hiyo iliyoanza Novemba 25 na kufikia tamati leo.
Uganda inashikilia rekodi ya kutwaa ubingwa huo mara nyingi zaidi ikiwa na imelibeba Kombe la Chalenji mara 11 wakati Rwanda imelitwaa mara moja tu mwaka 1999 wakati michuano hiyo ilipofanyika kwao jijini Kigali, ambapo iliifunga Kenya kwa magoli 3-1 katika mechi ya fainali.
Kama rekodi zina mchango wowote katika mechi za soka, Uganda itakuwa na nafasi kubwa zaidi ya kubeba kombe lao la 12 leo.
Mara zote mbili ambazo mataifa hayo yalikutana katika fainali za michuano hii, Uganda iliibuka mbabe. Katika michuano iliyofanyika nchini Sudan 2003, Uganda iliifunga Rwanda 2-0 katika fainali na kutwaa ubingwa kama ambavyo ilifanya pia mwaka 2009 nchini Kenya ilipowaangusha kwa ushindi kama huo katika fainali.
Huku Uganda ikiongoza ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati katika orodha ya FIFA ya viwango vya ubora wa soka duniani kwa kushika nafasi ya 91, Rwanda inashika nafasi ya 114.
Stars ambayo iliondolewa katika nusu fainali kwa kipigo cha 3-1 kutoka kwa Uganda itakuwa uwanjani kuwania dola 10,000 (Sh. milioni 16) dhidi ya Sudan ambayo iling'olewa na Rwanda 'Amavubi' kwa kipigo cha 2-1.
Akizungumzia mchezo huo, kocha msaidizi wa Kilimanjaro Stars Jamhuri Kihwelu 'Julio' alisema kuwa watafuta machozi ya mashabiki nyumbani kwa kushinda mechi yao ya mshindi wa tatu leo.
"Tumeondolewa kwenye hatua ya nusu fainali... hilo kwa sasa limepita na tunaangalia mchezo wa kesho (leo), tutashindana kupata ushindi wa tatu baada ya kuachia ubingwa wa mashindano haya," alisema Julio.
MUSONYE ASHUKURU
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicolaus Musonye alisema kuwa wanaishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwaunga mkono, kuruhusu mashindano hayo kufanyika nchini na kutoa Uwanja wa Taifa kwa ajili ya mashindano hayo.
Musonye alisema kuwa wananchi wa Tanzania wamekuwa mstari wa mbele kuwaunga mkono kwa kujitokeza kwenye mechi za mashindano hayo na hivyo kuifanya michuano kuwa hai.
Mashindano hayo mwakani yamepangwa kufanyika nchini Kenya ambapo nchi 14 zinatarajiwa kushiriki.
Miongoni mwa nchi ambazo si mwanachama wa CECAFA zinazotegemewa kushiriki mwakani ni Nigeria na Cameroon.
KAGAME YADHAMINIWA
Musonye alisema pia kuwa mashindano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati maarufu kama Kombe la Kagame yamepata mdhamini mpya ambaye yupo tayari kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kuyadhamini.
Alisema kuwa mwezi ujao uongozi wa CECAFA utakutana na mdhamini huyo mpya kwa ajili ya kujadili udhamini huo pamoja na kuchagua nchi itakayoandaa mashindano hayo kwa mwakani.
Mashindano hayo ambayo ubingwa wake unashikiliwa na mabingwa wa soka nchini Yanga, hushirikisha klabu bingwa kutoka kwa nchi mwanachama wa CECAFA pamoja na klabu mwalikwa kwa ajili ya kuleta changamoto.
Mashindano hayo mwaka jana yalifanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambapo timu za Tanzania za Simba na Yanga zilitinga hatua ya fainali.
No comments:
Post a Comment