Friday, December 9, 2011

Mourinho ‘auchuna’ Real wakiivaa Barca



MADRID, Hispania
KOCHA Jose Mourinho wa Real Madrid aliamua kutozungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa kawaida wa kabla ya mechi jana na msaidizi wake, Aitor Karanka, ndiye aliyetarajiwa kujibu maswali badala yake kuhusiana na mechi yao ya kwanza ya ‘Clasico’ watakayocheza nyumbani leo dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Barcelona, Real walisema kupitia tovuti yao (www.realmadrid.com).
Mourinho amekuwa na mahusiano mabaya na vyombo vya habari vya jiji la Madrid tangu alipotua akitokea Inter Milan mwishoni mwa msimu wa 2009-10 na alikataa kuzungumza kabla ya mechi yao ya La Liga dhidi ya Barca April na kusababaisha waandishi wa habari takribani 30 kuamua kutoka nje ya ukumbi. Kocha wa Barca, Pep Guardiola alitarajiwa kuzungumza na waandishi baadaye jana.
Huku takriban theluthi ya mechi za msimu zikiwa tayari zimeshachezwa, vinara Real wanaongoza kwa tofauti ya pointi tatu na pia wana mechi moja mkononi kulinganisha na Barca wanaowafuatia katika nafasi ya pili kwenye msimamo, ambao wanafukuzia rekodi ya klabu yao ya kutwaa ubingwa wa La Liga kwa mara ya nne mfululizo.
Real wameshinda katika mechi zao 10 zilizopita za La Liga, na mechi 15 mfululizo za michuano yote hadi sasa, wakati Barca wamefungwa katika mechi moja tu kati ya 11 za 'Clasicos' dhidi ya mahasimu wao wa jadi tangu Guardiola atwae madaraka mwaka 2008.
Kiungo huyo wa zamani wa Barca na timu ya taifa ya Hispania hajawahi kufungwa kwenye Uwanja wa Bernabeu akiwa kocha, akishinda mechi tatu na kupata sare mbili huku kikosi chake kikifunga mabao 13 na kuruhusu matano tu
Mourinho ana wakali wake wote kikosini isipokuwa beki wa kati wa kimataifa kutoka Ureno, Ricardo Carvalho, ambaye bado anauguza jeraha la goti na hajacheza tangu mwishoni mwa Septemba.
Guardiola pia ana wachezaji wake wote, ukiondoa Ibrahim Afellay, ambaye kwa muda mrefu sasa yuko nchini kwao Uholanzi akiuguza jeraha la goti alilofanyiwa upasuaji.

RATIBA YA LA LIGA (HISPANIA)
LEO, Jumamosi
Real Madrid v Barcelona (Saa 6:00) usiku
Levante v Sevilla (Saa 2:00) usiku
Betis v Valencia

RATIBA LIGI KUU ENGLAND
LEO Jumamosi
Arsenal v Everton (saa 12:00) jioni
Man U v Wolves (saa 12:00) jioni
Liverpool v QPR (saa 12:00) jioni
Bolton v Villa
Norwich v Newcastle
Swansea v Fulham
West Brom v Wigan

Kesho, Jumapili
Stoke v Tottenham (saa 1:00) usiku
Sunderland v Blackburn

KESHOKUTWA, Jumatatu
Chelsea v Man City (saa 5:00) usiku

Okwi, Niyonzima Nani Zaidi Chalenji?



UPINZANI wa wachezaji Emmanuel Okwi wa Uganda na Haruna Niyonzima wa Rwanda wanapokuwa katika klabu zao za Simba na Yanga, utarejea tena leo wakati mataifa hayo mawili yatakapopambana katika mechi ya fainali ya Kombe la Chalenji kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuanzia saa 9:15 alasiri.
Mechi hiyo itatanguliwa na pambano la kusaka mshindi wa tatu baina ya mabingwa wa mwaka jana Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars' dhidi ya Sudan litakaloanza saa 7:00 mchana. Awali michezo hiyo ilipangwa kuanza saa 8:00 mchana kwa mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu na saa 10:00 jioni kwa mchezo wa fainali lakini Baraza la Vyama vya Michezo la nchi za Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) jana lilirekebisha ratiba hizo.
Okwi, mbali na ushindani dhidi ya hasimu wake wa Yanga, Niyonzima, pia atakuwa akichuana na mshambuliaji ghali wa APR ya Rwanda, Olivier Karekezi mwenye magoli matano katika mbio za kuwania tuzo ya kiatu cha dhahabu ya mfungaji bora. Okwi ameifungia Uganda magoli manne katika michuano hiyo iliyoanza Novemba 25 na kufikia tamati leo.
Uganda inashikilia rekodi ya kutwaa ubingwa huo mara nyingi zaidi ikiwa na imelibeba Kombe la Chalenji mara 11 wakati Rwanda imelitwaa mara moja tu mwaka 1999 wakati michuano hiyo ilipofanyika kwao jijini Kigali, ambapo iliifunga Kenya kwa magoli 3-1 katika mechi ya fainali.
Kama rekodi zina mchango wowote katika mechi za soka, Uganda itakuwa na nafasi kubwa zaidi ya kubeba kombe lao la 12 leo.
Mara zote mbili ambazo mataifa hayo yalikutana katika fainali za michuano hii, Uganda iliibuka mbabe. Katika michuano iliyofanyika nchini Sudan 2003, Uganda iliifunga Rwanda 2-0 katika fainali na kutwaa ubingwa kama ambavyo ilifanya pia mwaka 2009 nchini Kenya ilipowaangusha kwa ushindi kama huo katika fainali.
Huku Uganda ikiongoza ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati katika orodha ya FIFA ya viwango vya ubora wa soka duniani kwa kushika nafasi ya 91, Rwanda inashika nafasi ya 114.
Stars ambayo iliondolewa katika nusu fainali kwa kipigo cha 3-1 kutoka kwa Uganda itakuwa uwanjani kuwania dola 10,000 (Sh. milioni 16) dhidi ya Sudan ambayo iling'olewa na Rwanda 'Amavubi' kwa kipigo cha 2-1.
Akizungumzia mchezo huo, kocha msaidizi wa Kilimanjaro Stars Jamhuri Kihwelu 'Julio' alisema kuwa watafuta machozi ya mashabiki nyumbani kwa kushinda mechi yao ya mshindi wa tatu leo.
"Tumeondolewa kwenye hatua ya nusu fainali... hilo kwa sasa limepita na tunaangalia mchezo wa kesho (leo), tutashindana kupata ushindi wa tatu baada ya kuachia ubingwa wa mashindano haya," alisema Julio.

MUSONYE ASHUKURU
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicolaus Musonye alisema kuwa wanaishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwaunga mkono, kuruhusu mashindano hayo kufanyika nchini na kutoa Uwanja wa Taifa kwa ajili ya mashindano hayo.
Musonye alisema kuwa wananchi wa Tanzania wamekuwa mstari wa mbele kuwaunga mkono kwa kujitokeza kwenye mechi za mashindano hayo na hivyo kuifanya michuano kuwa hai.
Mashindano hayo mwakani yamepangwa kufanyika nchini Kenya ambapo nchi 14 zinatarajiwa kushiriki.
Miongoni mwa nchi ambazo si mwanachama wa CECAFA zinazotegemewa kushiriki mwakani ni Nigeria na Cameroon.

KAGAME YADHAMINIWA
Musonye alisema pia kuwa mashindano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati maarufu kama Kombe la Kagame yamepata mdhamini mpya ambaye yupo tayari kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kuyadhamini.
Alisema kuwa mwezi ujao uongozi wa CECAFA utakutana na mdhamini huyo mpya kwa ajili ya kujadili udhamini huo pamoja na kuchagua nchi itakayoandaa mashindano hayo kwa mwakani.
Mashindano hayo ambayo ubingwa wake unashikiliwa na mabingwa wa soka nchini Yanga, hushirikisha klabu bingwa kutoka kwa nchi mwanachama wa CECAFA pamoja na klabu mwalikwa kwa ajili ya kuleta changamoto.
Mashindano hayo mwaka jana yalifanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambapo timu za Tanzania za Simba na Yanga zilitinga hatua ya fainali.

Kanumba sasa ni Big Daddy



BAADA ya kutamba na 'Because of You', nyota wa filamu nchini, Steven Kanumba 'The Great', anajiandaa kupakua kazi nyingine mpya itwayo 'Big Daddy'.
Filamu hiyo mpya ya Kanumba, imewashirikisha wasanii tofauti wakiwemo wakongwe na chipukizi ambao wamefanya kazi kubwa, kwa sasa ipo kwenye foleni kabla ya kuachiwa sokoni.
Kwa mujibu wa Kanumba, kazi hiyo yenye ubora wa hali ya juu itaingia sokoni wiki tatu zijazo, ingawa yupo 'chimbo' kuandaa kazi nyingine kwa ajili ya kufungia mwaka.
Mbali ya Kanumba, ndani ya filamu hiyo amecheza na wasanii kama Jamila Jaylawi, Jalilah Jaylawi, Cathy Rupia, Abdul Ahmed, Patchou Mwamba na wengine.
"Si kazi ya kuikosa kuiona kwa namna simulizi lake lilivyo na inavyosisimua," alisema Kanumba.
Katika hatua nyingine, msanii mwingine mkali wa fani hiyo, Mohammed Nurdin 'Chekibud' amepakua kazi iitwayo Azma ambayo inatarajiwa kutoka katikati ya mwezi huu ikiwashirikisha nyota kadhaa akiwemo Kulwa Kikumba 'Dude'.
Filamu hiyo inayohusiana na mambo ya mapenzi, ipo foleni kabla ya kuingizwa sokoni, pia imewashirikisha waigizaji kama Zuwena Mohammed 'Shilole', Snura Mushi na wengine.
Chekibud, amewataka mashabiki wake kujiandaa kuishuhudia kazi hiyo aliyodai ni moja kati ya filamu za kufungia mwaka 2011 kutokana na ubora iliyonayo kuanzia hadithi, mandhari na washiriki walivyoicheza.

Ally Akida achukuliwa Extra Bongo





BAADA ya kimya cha muda mrefu hatimaye mmoja wa wanamuziki waanzilishi wa bendi ya Twanga Pepeta, Ally Akida, amejiunga na bendi inayokuja kwa kasi katika anga za muziki wa dansi ya Extra Bongo.
Mkurugenzi wa bendi hiyo, Ally Choki alisema kuwa amemuongeza Akida kwa vile ni mwanamuziki kiraka ambaye anamudu kupiga gita lolote na kwamba hata mmoja anapopata dharura kazi itaendelea kama kawaida.
"Ninaujua uwezo wa Ally Akida ndio maana tumemchukua ili ajiunge na bendi yetu, kwani kwa muda mrefu kidogo alikuwa anafanya shughuli zake tu baada ya kuachana na Twanga Pepeta," alisema Choki.
Alisema kwamba atakuwa na msaada mkubwa kwenye bendi hiyo ambayo kwa sasa inaendelea na kazi ya kujitambulisha ndani na nje ya Dar es Salaam huku pia ikiwa mbioni kukamilisha albamu ya pili.
Alisema kuwa ingawa mwanamuziki huyo hajambulishwa rasmi kwa wapenzi wa bendi hiyo, ana uhakika kwamba wale ambao wamekuwa wakihudhuria maonyesho ya Extra Bongo wameshamuona akifanya vitu vyake.
"Tuna sababu zetu za msingi za kutomtambulisha rasmi, lakini wakati mufaka ukifika tutafanya mara baada ya kukamilisha mipango ya kuongeza wanamuziki wengine kazi ambayo bado inaendelea,"alisema.
Alifafanua kuwa mipango hiyo ikikamilika, Extra Bongo itawatambulisha wanamuziki wote wapya akiwemo Ally Akida aliyejiunga na bendi hiyo hivi karibuni ikiwemo pia mpiga tumba mpya John Ngosha.
John Ngosha ni mtoto wa mwanamuziki wa zamani wa bendi ya DDC Mlimani Park 'Sikinde', Charles marehemu John Ngosha.
Extra Bongo ilianza kwa albamu ya 'Mjini Mipango' na sasa imekamilisha nyimbo za albamu ya pili zikiwemo za 'Fisadi wa Mapenzi', 'Watu na Falsafa', 'Mtenda Akitendewa', 'Mashuu', 'Neema' na nyinyine nyingi.
Nyimbo hizo zimekuwa zikiporomoshwa kwenye maonyesho ya bendi hiyo likiwemo la kila Jumamosi ambalo hufanyika katika ukumbi wa Meeda Club uliopo Sinza-Mori, jijini Dar es Salaam.

Steps kumtoa Makassy kwenye injili




KAMPUNI ya usambazaji wa filamu nchini ya Steps Entertainment imejitosa kwenye muziki wa Injili na sasa iko mbioni kutoa DVD mbili za miondoko hiyo moja ikimjumuisha nyota wa zamani wa dansi, Kitenzogu Makassy 'Mzee Makassy'.
Mkongwe huyo aliyetamba na bendi mbalimbali za dansi ikiwemo Makassy Band, kwa muda mrefu amejitosa kwenye muziki wa Injili, ambapo Steps imeijumuisha kazi yake katika DVD iitwayo Amen Gospel Colletion inayotarajiwa kutoka sambamba na Ebenezer Collection Vol.1.
Kwa mujibu wa Steps, DVD hizo kila moja itakuwa na jumla ya nyimbo tisa za nyota wa miondoko hiyo wakiwemo Jane Misso, Christina Shusho, Bonny Mwaitege na wengineo.
Taarifa ya Steps inasema katika DVD ya Amen, mbali na Mzee Makassy, albamu hiyo ina nyimbo kama 'Hakuna kama Yesu' wa Christina Shusho, 'Lango ni Yesu'- Jane Misso, 'Mimi Siyawezi-Abedy Ngosha na 'Bwana ndio Mchungaji' ulioimbwa na Solomoni Mukubwa.
Katika albamu ya pili ya Ebenezer Collection Vol.1, ina nyimbo za wakali kama Bonny Mwaitege, Abiud Mashari, Neema Mwaipopo, Ambwene Mwasongwe na wengineo na zote zintarajiwa kutoka kabla ya sikukuu ya Krismasi.
"Steps tupo mbioni kuingiza mtaani albamu mbili za muziki wa Injili zinazohusisha nyota wa miondoko hiyo zitakazokuwa na nyimbo tisa kila mmoja, ambapo moja inafahamika kwa jina la Amen Gospel Collection na nyingine Ebenezer Collection Vol. 1," taarifa hiyo ya Steps inasomeka hivyo.